Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Aamuru Wananchi wa Kijiji Kizima Wakamatwe na Kuwekwa Ndani.....RPC Mbeya Tayari Keshatuma Polisi

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila, ameliagiza Jeshi la Polisi kuwakamata na kuwasweka ndani wananchi wote wa Kijiji cha Ngole kilichopo Kata ya Ilungu wilayani Mbeya kwa kosa la kuharibu mradi wa maji wa kijiji jirani cha Msheye.

Wananchi hao wanadaiwa kuvamia na kuharibu mradi huo kwa kuvunja banio na kukata mabomba yaliyokuwa yametandazwa kuanzia kwenye chanzo cha maji kwenda kwenye makazi ya kijiji jirani wakitumia vifaa mbalimbali yakiwamo majembe na mapanga.

Ametoa agizo la kukamatwa wananchi hao jana wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya walioketi kupokea na kujadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Aidha, amefikia uamuzi huo mara baada ya Mwenyekiti wa Kijiji cha Mashesye, Osiah Mwakalila, kuwasilisha taarifa juu ya unyama waliofanyiwa na majirani zao, akidai kuwa pia walikuwa wanatishia kuwashambulia endapo wangeendelea kuhoji na kuwazuia kutekeleza uamuzi wao.

“Naagiza wananchi wote wa kijiji hicho wakamatwe wawekwe ndani bila kujali ana hali gani, watajieleza wakiwa ndani, haiwezekani sehemu zingine watu wanahangaika maji huku sehemu nyingine watu wanafyeka mabomba,” amesema Chalamila

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei, amesema magari yameshatumwa yakiwa na askari wa kutosha kwa ajili ya kuwakamata wananchi hao.

Amesema kitendo kilichofanywa na wananchi wa Kijiji hicho ni uhujumu uchumi hivyo lazima washughulikiwe ipasavyo.



from MPEKUZI

Comments